Sunday 22 October 2017

Matumizi ya Kadi za Benki katika Manunuzi Kwenye Mtandao

matumizi-ya-kadi-za-benki
Teknolojia inayowezesha matumizi ya kadi za benki kununua bidhaa katika maduka na mtandao wa kompyuta ni kitu kilichozoeleka na kufanyika sana katika nchi zilizoendelea hasa Ulaya na Marekani.
Lakini kwa Afrika ikiwemo Tanzania si jambo la kawaida sana. Japo kuna watu wachace ambao wanatumia.
Kuna fursa nyingi katika utumiaji wa kadi za benki kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma,ikiwemo kununua bidhaa toka nje kwa bei nafuu ukilinganisha na kununua kwa wachuuzi wa maduka.
Bidhaa hasa za kielektroniki kama vitabu na programu za kompyuta au simu zinapatikana kwa urahisi kutoka katika masoko kupitia mtandao wa kompyuta.
Biadhaa nyingine ni zile halisi kama kamera,simu,komputa,vitabu na vingine vingi kutaja vichache vinaweza vikanunuliwa toka maduka ya nje ya nchi kwa bei nafuu na vyenye ubora mkubwa.

Kadi za Benki ni nini?

Hizi ni kadi za kuchukulia fedha katika mashine ya kutoa fedha(ATM) ambazo zinakuwezesha pia kununua bidhaa na huduma katika sehemu za mauzo kama mahotelini,maduka ya bidhaa(“Supermarkets”) na katika masoko ya kwenye matandao wa intaneti.
Kadi hizi zimeunganishwa na akaunti yako ya benki na kila unaponunua kupitia kadi hii kiasi cha fedha kinapunguzwa katika akaunti yako sawa na ghramaya bidhaa iliyonunuliwa.
Makampuni ya Benki yanafanya kazi na makampuni ya kimataifa ambayo yanawezesha mfumo huu wa manunuzi kufanya kazi kokote duniani. Baadhi ya makampuni makubwa duniani ni MasterCard na VISA
matumizi-ya-kadi-za-benki_mastercard
Kadi ya MasterCard
matumizi-ya-kadi-za-benki_visa
Kadi ya VISA
 Aina za Kadi:
Kuna aina mbili za kadi za manunuzi
i. Kadi za Malipo ya Mkopo-Creditcard:
Kadi hizi zinaruhusu mteja kununua hata kama hana fedha za kutosha katika akaunti yake na atarudisha mkopo baada ya muda ambao atapangiwa au fedha nyingine inapokuwa imeingia kwenye akaunti hiyo.
Aina hii ya kadi zinatumika zaidi katika nchi zilizoendelea,na aghalabu hutolewa na benki nchini Tanzania.
ii. Kadi za Malipo ya Awali-Debitcard:
Kadi hizi zinamuwezesha mteja kununua kama tu kuna fedha za kutosha katika akaunti yake vinginevyo manunuzi hayatawezekana.
Aina hii ya kadi ndizo ambazo zinatolewa kwa wingi nchini Tanzania.

Matumizi ya kadi za Benki katika Manunuzi:

Nchini Tanzania kwa sasa karibu kadi zote za benki zimeunganishwa na huduma hii na inawawezesha wateja wake wote wenye Kadi za MasterCard au VISA kuweza kununua katika mtandao na katika mashine zilizopo katika maduka na sehemu za huduma mbalimbali kama mahotelini. Pia kadi hizi zinawezesha wateja kutoa fedha katika mashine za fedha (ATM) zozote duniani na kuwawezesha wasafiri kutembea bila fedha wanapokuwa ndani na nje ya nchi.
matumizi-ya-kadi-za-benki_pos-1
Matumizi ya kadi za benki inatoa fursa kwa wafanyabiashara mbalimbali nchini Tanzania na nchi nyingine za Africa kuunganisha machine za malipo ambazo zinaweza kusoma kadi za benki na kurahisisha namna biashara zinanyofanyika.
Huduma za manunuzi ya umeme,mafuta katika vituo vya kuuza mafuta,maduka na hata ulipaji wa kodi mbalimbali. Utumiaji wa mfumo huu katika sehemu za huduma itasaidia kupunguza msongamano wa watu katika sehemu hizi za utoaji huduma kwa jamii.
Pia matumizi ya mfumo huu yatasaidia kupunguza hatari ya kutembea na fedha nyingi na kuvutia wezi barabani na nyumbani.

Faida za Matumizi ya Kadi za Benki Katika Manunuzi

i. Urahisi wa Kupata Huduma
Kutumia kadi kunarahisisha kupata huduma mahala popote, wakati wowote.
Hakuna sababu ya kwenda benki na kusimama katika mstari mrefu.
ii. Unafuu wa Bei
Kwa baadhi ya bidhaa hasa toka nje ya nchi zinaweza kupatikana kwa bei nafuu zaidi kuliko ukinunua toka dukani nchini kwako. Mfano ukinunua kitabu toka Amazon utapata kwa bei nafuu kuliko kununua katika duka la vitabu nchini Tanzania. Hii ni kutokana na gharama za kodi na usambazaji za wauzaji.
 iii. Kupunguza Wizi wa Fedha Taslimu
Ukitumia kadi kwa manunuzi huhitaji kutembea na fedha nyingi mfukoni hivyo kupunguza hatari ya kupoteza au kuibiwa.
iv. Usumbufu wa Kutembea na Fedha Taslimu
Matumizi ya kadi yanaondoa usumbufu wa kutembea na fedha nyingi mfukoni au kutunza majumbani.

 Na Hasara Je?

Kama ilivyo kwa vitu vingine vingi vizuri pia havikosi ubaya kwa upande wa pili:
i. Hatari ya Wizi wa Mtandao
Kumekuwa na matukio ya wizi wa fedha kupitia mtandao na kutumia kadi yako kwa manunuzi kwa jinsi isiyo salama inaongeza hatari ya kuibiwa na wezi katika mtandao.
Hili linaweza kudhubitiwa kwa kuhakikisha unafuata sawa sawa masharti ya usalama kama vile kutogawa namba ya siri kwa yeyote na kutunza kadi sehemu iliyo salama.
 ii. Utegemezi Katika Uwepo wa Mtandao
Kwakuwa kazi zinatumia mtandao kunafanya ukose huduma kama mtandao unakuwa umekatika. Hii inaweza ikakuchelewesha kupata huduma stahiki kwa wakati.
 iii. Kutumia Fedha Kupita Kiasi
Matumizi ya kadi katika manunuzi yanaweza yakakushawishi kutumia zaidi kuliko kama ungetumia fedha taslimu. Hivyo ni muhimu kukuwa na bajeti na kuifuta.
iv. Gharama za Ziada
Kuna gharama za kufanya mwamala katika mtandao ambazo wakati mwingine zinaweza zikafanya bei kuwa kubwa kidogo kuliko kama ungetumia fedha taslimu.

Muda wa Kuhama Umefika?

Bila shaka wakati umefika sasa kwa waafrika kuhamia katika teknolojia hii ya benki,kuna idadi kubwa tayari wanatumia kadi hizi nikiwemo mimi mwenyewe na inaleta mapinduzi makubwa sana kwenye urahisi wa manunuzi na matumizi mazuri ya muda.
Matumizi ya kadi za benki katika mfumo wa manunuzi na malipo itaboresha sekta ya biashara na hata kwa wakulima wa vijijini ambako mtandao wa intaneti umefika au unaweza kufika wataweza kufaidika nayo pia.
Afrika na mataifa yake inapaswa kufahamu kuwa matumizi ya teknolojia kwa njia iliyo sahihi inasaidia sana maendeleo ya nchi kama ambavyo imetokea katika nchi zilizoendelea.
Kama serikali ikitengeneza mfumo mzuri katika taasisi zake kama TRA,Wizara ya fedha,TANESCO na mashirika mengine ya huduma na udhibiti wa fedha ikiwemo benki kuu mfumo huu unaweza ukatumika katika biashara nchini na kuongeza tija na ufanisi.

No comments:

Post a Comment